jinsi ya kupata Green Card
Green Card, ambayo inajulikana pia kama kadi ya mkazi wa kudumu, inakuwezesha kuishi na kufanya kazi nchini Marekani daima. Pata taarifa kuhusiana na njia za kupata Green Card. Fahamu hatua za kutuma maombi na jinsi ya kujiandaa kwa mahojiano yako.
Green Card ni nini?
Green Card inawawezesha watu ambao si raia wa Marekani kuishi na kufanya kazi nchini Marekani. Ni hati ya utambulisho yenye jina lako na picha yako.
Green Card ni uthibitisho wa hali yako ya uhamiaji kama mkazi halali wa kudumu (LPR).
Green Card nyingi ni halali kwa miaka 10. Ukiwa mkazi mwenye masharti, ni halali kwa miaka 2.Green Card pia inaitwa kadi ya mkazi wa kudumu.
Faida za kuwa na Green Card
Ukiwa na hali ya mkazi wa kudumu unaweza:
- kuishi na kufanya kazi nchini Marekani daima bila hofu ya kuwekwa kizuizini au kufukuzwa nchini
- kusafiri nje ya Marekani kwa hadi miezi 12
- kupokea mafao ya serikali kuu, kama vile usaidizi wa kulipia elimu na makazi
- kuomba kuleta wanafamilia wako Marekani
- kuomba uraia wa Marekani baada ya miaka 5
Nani anaweza kutuma maombi?
Kuna njia mbalimbali unaweza kuwa mkazi halali wa kudumu. Unaweza kutuma maombi ikiwa upo katika kategoria inayostahiki:
Wanafamilia wa raia wa Marekani au wamiliki wa Green Card
- Raia wa Marekani wanaweza kufadhili wazazi wao, wenzi wao, wachumba wao, watoto ambao hawajaolewa, na kaka au dada ambao ni watu wazima. Mtu ambaye ni mjane wa raia wa Marekani anaweza pia kutuma maombi.
- Wamiliki wa Green Card wanaweza kuwafadhili wenzi wao na watoto wasio na ndoa kwa ajili ya ukazi wa kudumu.
- Raia wa Marekani na wamiliki wa Green Card hawawezi kufadhili wanafamilia baki kama binamu, mashangazi, wajomba na bibi na babu.
Baadhi ya wafanyakazi
Green Card kwa wahamiaji wa kuajiriwa inapatikana kwa baadhi ya wafanyakazi, madaktari na wawekezaji.
Wahamiaji maalum
Wafanyakazi wa kidini, vijana wahamiaji maalum, wafasiri au wakalimani wa Kiafghanistan au Kiiraki waliofanya kazi na serikali ya Marekani, wanahabari na wafanyakazi wa mashirika ya kimataifa wanaweza kutuma maombi.
Wakimbizi na watafuta hifadhi
Wakimbizi na watafuta hifadhi wanaweza kutuma maombi ya Green Card mwaka mmoja baada ya kupokea hali yao.
Mhanga wa unyanyasaji, uhalifu na biashara haramu ya binadamu
Baadhi ya wahanga wa unyanyasaji wanaweza kutuma maombi chini ya VAWA, Hali ya Vijana Wahamiaji Maalum, Sheria ya Urekebishaji ya Cuba, na Sheria ya Haki ya Wahamiaji wa Haiti. Wahanga wa biashara haramu ya binadamu na wahanga wengine wa uhalifu wanaweza pia kutuma maombi.
Wakazi wa muda mrefu
Ikiwa umeishi Marekani tangu Januari 1, 1972, unaweza kutuma maombi. Hii inaitwa Green Card kupitia rejesta. Hili linaweza kuwa chaguo hata kama huna vibali au umeishi Marekani kinyume cha sheria.
Watu wengine wasio wahamiaji
Baadhi ya watu wanaweza kuomba Green Card chini ya programu nyingine zikiwemo:
- Haki ya Uhamiaji kwa Wakimbizi wa Liberia (LRIF)
- Programu Anuai ya Visa ya Wahamiaji (bahati nasibu ya Green Card)
- Sheria ya Urekebishaji ya Cuba
- Hali ya utegemezi chini ya HRIFA
- Lautenberg parolee
- Sheria ya Urekebishaji Parole ya Indochina ya mwaka 2000
- Muhindi Mwamerika mzaliwa wa Kanada
- Mwanadiplomasia au mtu aliyezaliwa Marekani na mwanadiplomasia wa kigeni
Matakwa
Kila kategoria ya ustahiki wa Green Card ina matakwa mahsusi ambayo lazima uyatimize.
Ikiwa upo Marekani
Afisa wa uhamiaji lazima awe amekukagua na kukuruhusu wakati unapoingia Marekani. Kutuma maombi ndani ya Marekani kunajulikana rasmi kama urekebishaji wa hali.
Ukiwa nje ya Marekani
Ni lazima uombe visa ya wahamiaji kwenye ubalozi wako mahalia ili kuja Marekani. Utaratibu huu unajulikana rasmi kama mchakato wa kibalozi.
Sheria ya usaidizi wa umma (public charge) hairuhusu watu watakaotegemea usaidizi fulani wa serikali kupata Greeen Card. Watafuta hifadhi, wakimbizi, walioachiliwa kwa msamaha wa masuala ya kibinadamu, na wahanga wa biashara haramu ya binadamu na uhalifu hawaguswi na sheria hii. |
Jinsi ya kutuma maombi
Kwa kuwa sasa umekagua kategoria tofauti, hizi hapa ni hatua zinazofuata za kuchukua:
Hatua ya 1: Hakikisha kama unastahiki kutuma maombi
- Kila kategoria ya Green Card ina matakwa mahsusi.
Hatua ya 2: Ukiweza tafuta usaidizi wa kisheria
- Daima inasaidia kupata usaidizi wa kisheria unapojaribu kurekebisha hali yako ya uhamiaji. Kuna mashirika na wanasheria wengi wanaotoa hutoa usaidizi bila malipo au kwa gharama ndogo.
Hatua ya 3: Fahamu kama unapaswa kuomba visa
- Mwanafamilia wako anaweza kulazimika kuwasilisha Fomu I-130 na hati ya kiapo ya utegemezi kwa Huduma za Uraia na Uhamiaji Marekani (USCIS).
- Mwajiri wako anaweza kulazimika kuwasilisha Fomu I-140 kwa USCIS.
Hatua ya 4: Wasilisha maombi yako
- Ukiwa nje ya Marekani, lazima uombe visa ya wahamiaji kwenye ubalozi wako mahalia ili kuja Marekani.
- Ukiwa ndani ya Marekani, lazima uwasilishe Fomu I-485 kwa USCIS.
- Lazima pia ufanye uchunguzi wa kitiba na ujumuishe Fomu I-693 pamoja na maombi yako ya Green Card.
- Fuata vidokezo vya kuwasilisha maombi yako ya Green Card.
- Lipa ada zako za kuwasilisha maombi. Zinatofautiana kulingana na umri. Tumia kikokotoo cha ada cha USCIS.
- Kumbuka: unaweza pia kutuma maombi ya “social security number’ kwa wakati mmoja.
Hatua ya 5: Miadi yako ya taarifa za biometriki
- Waombaji wa Green Card wenye kati ya umri wa miaka 14 na 78 wanatakiwa kutoa taarifa za biometriki. Fahamu kuhusu nini cha kutarajia katika miadi yako.
Hatua ya 6: Mahojiano yako kuhusu Green Card
- Watu wengi watalazimika kuhojiwa katika ofisi mahalia ya USCIS. Afisa wa uhamiaji atakagua majibu ya maombi yako. Anaweza pia kuuliza maswali mengine ili kuamua kama unastahiki kupewa Green Card.
Hatua ya 7: Pata majibu ya maombi yako
- Afisa wa uhamiaji au afisa wa ubalozi atatoa uamuzi kuhusu maombi yako mwishoni mwa mahojiano yako. Katika baadhi ya matukio, afisa anaweza kuomba ushahidi zaidi kabla ya kutoa uamuzi.
- Maombi yako yakiidhinishwa, utapokea barua nyingine yenye Green Card yako.
- Maombi yako yakikataliwa, utapata maelezo kuhusu uwezekano wako wa kukata rufani.
Hatua ya 8: Kupewa Green Card yako
- Muda wa kusubiri Green Card unategemea kategoria na eneo ambalo umetuma maombi. Unaweza kutafuta makadirio ya muda wa mchakato mtandaoni.
Unaweza kuangalia hali ya maombi yako mtandaoni au kwa kupiga simu Kituo cha Mawasiliano cha USCIS.
Mahojiano kuhusu Green Card
Kuna mambo kadhaa unayoweza kufanya ili kujiandaa kwa mahojiano.
- Kagua maombi yako kabla ya mahojiano yako. Fanya maandalizi na wakili, wakala wa makazi mapya, familia, au rafiki.
- Njoo na nakala ya maombi yako.
- Njoo na hati halisi za nyaraka zote zinazounga mkono maombi yako ikiwemo pasipoti yako, hati ya kusafiria na Fomu I-94.
- Hakikisha unajibu maswali yote kwa ukweli.
- Njoo na mkalimani wako mwenyewe ikiwa unamhitaj na ujaze Fomu G-1256. Mkalimani wako lazima awe na angalau miaka 18, anayeongea lugha yako na Kiingereza kwa ufasaha, na asijihusishe na suala lako.
Taarifa kwa wamiliki wa Green Card
Unaweza kuwasilisha ombi la kuondoa masharti kwenye Green Card yako ya miaka 2, siku 90 kabla ya muda wake kuisha.
- Ukiwa na Green Card ya familia, wasilisha Fomu I-751. Utalazimika kuthibitisha kwamba ulifunga ndoa kwa nia njema, ikimaanisha ndoa yako ni ya kweli.
- Ukiwa na Green Card inayohusiana na kazi, wasilisha Fomu I-829. Utalazimika kuthibitisha kwamba umewekeza au unawekeza $1,050,000 katika biashara mpya na ajira 10 za kudumu.
- Ukiwasilisha mojawapo ya fomu hizi, Green Card yako itaendelea kuwa halali kwa muda wa miezi 48 baada ya tarehe ya muda wake kuisha.
Unapaswa kuifufua miezi sita kabla ya muda wake kuisha. Kadi yako ikipotea, ikiibiwa, au ikiharibika, unaweza kubadilishiwa.
Wasilisha Fomu I-90 ili kufufua au kubadilisha kadi yako. Unaweza kuwasilisha maombi yako mtandaoni au kwa njia ya posta.
Ukiwasilisha Fomu I-90 ili kufufua Green Card inayokaribia au iliyoisha muda wake, Green Card yako itaendelea kuwa halali kwa miezi 24 huku USCIS ikishughulikia maonbi yako. Unaweza kutumia stakabadhi yako kama ushahidi wa muda wa hali yako ya mkazi halali wa kudumu.
Ikiwa unasubiri kubadilishiwa Green Card, unaweza kuwasiliana na ofisi ya USCIS iliyo karibu nawe ili kuomba uthibitisho wa hali yako ya Green Card.
Usaidizi wa umma hauhusiki kwako ikiwa unaomba kufufua Green Card yako. Huenda ukalazimika kupitia mchakato mwingine wa ubainifu wa kukataliwa usaidizi wa umma ikiwa utarejea Marekani baada ya kutokuwepo kwa zaidi ya siku 180.
Utahitaji kuonesha pasipoti au hati ya kusafiria unapotoka Marekani. Utahitaji kuonesha Green Card yako unaporudi Marekani. Ukisafiri nje ya Marekani kwa zaidi ya mwaka mmoja, lazima uombe kibali cha kuingia tena Marekani. Unaweza kuwasilisha Fomu I-131.
Elewa jinsi ya kujilinda dhidi ya wanasheria feki (notarios) na tovuti bandia. Fahamu nini cha kufanya ikiwa umekuwa mhanga wa ulaghai.
Taarifa kwenye ukurasa huu umetoka kwa USCIS na vyanzo vingine vinavyoaminika. Malengo yetu ni kutoa taarifa zilizo rahisi kuelewa na zinazosasishwa mara kwa mara. Taarifa hii si ushauri wa kisheria.