Mafao ya wahamiaji na huduma za wakimbizi
Je, unapata wakati mgumu kulipia gharama za msingi za maisha? Mafao ya umma na huduma kutoka serikali ya Marekani zinaweza kusaidia. Fahamu chaguzi zilizopo kwa wahamiaji na wakimbizi na jinsi ya kuomba.
Mafao ya umma ni nini?
Serikali ya Marekani inatoa mafao ya umma kwa huduma muhimu, ikiwemo chakula, makazi, huduma za afya na elimu. Mashirika ya huduma za kijamii yanaendesha programu hizi za serikali kuu. Yanasaidia:
- Watu wenye kipato cha chini
- Watu wasio na makazi
- Watu wenye ulemavu
Mafao mengi ya umma yanategemea kipato chako na ukubwa wa familia. Yanakusudiwa kukusaidia kwa muda. Kiasi cha usaidizi unaopata kinaweza kupungua au kukoma mara tu unapotengeneza pesa zaidi.
Kila jimbo lina programu yake hivyo mafao ya umma hutofautiana kati ya jimbo na jimbo. Ukihama, kwa kawaida utahitaji kuomba upya usaidizi katika jimbo lako jipya.
Wakimbizi, watafuta hifadhi, na wahamiaji wanaweza pia kustahiki huduma za ziada za Ofisi ya Makazi Mapya ya Wakimbizi (ORR). |
Nani anaweza kupata mafao ya umma?
Raia wa Marekani na baadhi ya wahamiaji wenye sifa wanastahiki mafao ya umma. Wahamiaji wenye sifa wanajumuisha:
- Wakazi halali wa kudumu (wenye Green Card)
- Wakimbizi na watafuta hifadhi
- Wageni wa Cuba na Haiti
- Wenye visa maalum ya wahamiaji
- Wahanga wa biashara haramu ya binadamu
- Wasamehewa wa masuala ya kibinadamu
Ustahiki pia unategemea matakwa mahsusi ya jimbo. Kila jimbo lina sheria zake. Baadhi ya majimbo hutoa mafao ya umma kama vile bima ya afya kwa wakazi wote, bila kujali hali ya uhamiaji.
Wahamiaji wasio na vibali na wengine ambao hawajaorodheshwa kwa ujumla hawastahiki mengi ya mafao ya umma. Hata hivyo, wanaweza kupokea usaidizi kutoka mashirika ya huduma za jamii na programu za jumuiya.
Shirika la huduma za kijamii la eneo lako linaweza kujibu maswali yoyote uliyonayo. Benefits.gov ina mafao kulingana na jimbo. |
Aina za mafao ya umma ni zipi?
Usaidizi wa Muda kwa Familia zenye Uhitaji (TANF)
TANF (inayojulikana pia kama ustawi) hutoa pesa kwa familia za kipato cha chini. Programu hii husaidia kulipia chakula, makazi, malezi ya watoto na mafunzo ya ajira. Utapewa mafao ya TANF kupitia kadi ya benki, amana ya moja kwa moja, au hundi za karatasi kulingana na jimbo lako.
Ni muhimu kujua kwamba kiasi cha usaidizi unaopokea kinaweza kuwa tofauti sana na mtu aliye katika jimbo tofauti. Kila jimbo lina kiasi chake kulingana na ukubwa wa kaya na kipato.
Jinsi ya kuomba: Wasiliana na programu ya TANF ya eneo lako kwa maelezo kuhusu matakwa ya ustahiki na jinsi ya kuomba.
Kipato cha Usalama cha Ziada (SSI)
SSI hutoa malipo kila mwezi kwa wazee wenye miaka 65 au zaidi waliostaafu na hawafanyi kazi tena, au wanapata kiasi kidogo kila mwezi. Kiasi cha malipo ya kila mwezi kinatofautiana kulingana na kipato, rasilimali na hali ya maisha.
Pata maelezo ya SSI katika lugha nyingi.
Jinsi ya kuomba: Jaza ombi la mtandaoni. Unaweza pia kupiga simu ya usaidizi ya SSI kupitia 1-800-772-1213. Utapewa miadi kwa ajili ya kukamilisha ombi lako.
Bima ya Ulemavu ya ‘Social Security’ (SSDI)
SSDI hutoa kipato kwa watu wenye ulemavu ambao unapunguza au kuzuia uwezo wao wa kufanya kazi kwa mwaka au zaidi. Malipo yako ya kila mwezi yanategemea historia yako ya kazi. Pia utapata kinga ya bima ya afya kupitia Medicare.
Medicaid
Medicaid hutoa bima ya afya ya bure au ya gharama nafuu kwa wazee, watu wenye ulemavu, watoto, wanawake wajawazito, na familia za kipato cha chini. Wahamiaji wengi lazima wasubiri miaka 5 baada ya kupokea hali ya uhamiaji kabla ya kuomba Medicaid. Wakimbizi na watafuta hifadhi hawasubiri.
Medicaid ya Dharura hulipia huduma za dharura, ikiwemo kuwepo hospitalini. Medicaid ya Dharura inapatikana kwa wahamiaji wasiochukuliwa kama “watu wasio raia wenye sifa” ila wanakidhi sheria zote za jimbo za kipato na ukazi. Wahamiaji wasio na vibali wanaweza kuomba Medicaid ya Dharura.
Jinsi ya kuomba: Jaza ombi katika Health Insurance Marketplace. Unaweza pia kuangalia shirika la Medicaid la jimbo lako kwa maelezo ya ustahiki na jinsi ya kuomba.
Programu ya Bima ya Afya ya Watoto (CHIP)
Programu ya Bima ya Afya ya Watoto (CHIP) hutoa huduma ya afya ya bure au ya gharama nafuu kwa watoto na wajawazito. Hii ni kwa ajili ya familia ambazo hupata pesa nyingi sana na hivyo kutostahiki Medicaid. Katika baadhi ya majimbo, lazima usubiri miaka 5 baada ya kupata hali ya uhamiaji ndipo ujiandikishe na CHIP.
Jinsi ya kuomba: Jaza ombi katika Health Insurance Marketplace. Pata maelezo zaidi kuhusu programu ya CHIP katika jimbo lako.
Medicare
Medicare hutoa bima ya afya ya bure au gharama nafuu kwa wazee wenye miaka 65 au zaidi na wenye ulemavu na magonjwa hatari.
Jinsi ya kuomba: Jaza ombi la mtandaoni la Medicare. Unaweza kujiandikisha na Medicare wakati unajiandikisha na mafao ya “Social Security’ au unapostaafu. Piga simu ya Medicare kupitia 1-800-633-4227 kwa usaidizi katika lugha yako.
Programu ya Usaidizi wa Lishe ya Ziada (SNAP)
SNAP (food stamps) husaidia familia za kipato cha chini kununua chakula kupitia kadi. Utapata mafao ya SNAP kwenye kadi ya Uhamishaji Mafao Kielektroniki (EBT). Inafanya kazi kama kadi ya benki.
Kila mwezi, unapata kiasi fulani cha pesa kwenye kadi yako. Unaweza kutumia kadi hiyo kununua chakula katika maduka yaliyoidhinishwa. Ni lazima utimize matakwa fulani ya kipato na kazi ili ustahiki SNAP.
Iwapo wewe si raia wa Marekani, lazima pia ukidhi angalau 1 kati ya yafuatayo ili upate sifa:
- Umeishi Marekani kwa miaka 5+
- Unapata mafao yanayohusiana na ulemavu
- Una miaka chini ya 18
Jinsi ya kuomba: Wasiliana na ofisi ya SNAP ya jimbo lako kwa taarifa ya jinsi ya kuomba.
Iwapo hustahiki SNAP au haikidhi mahitaji yako, ghala za chakula (food pantries) hutoa chakula cha bure na kwa kawaida huwa wazi kwa yeyote anayehitaji. |
Programu Maalum ya Lishe ya Ziada kwa Wanawake, Wachanga na Watoto (WIC)
WIC huwasaidia wanawake wajawazito na wanaonyonyesha na watoto chini ya miaka 5 kupata chakula, ushauri nasaha wa lishe, na rufaa kwa huduma za kijamii. Lazima ukidhi matakwa fulani ya kipato na afya ili upate sifa.
Jinsi ya kuomba: Wasiliana na shirika la WIC la jimbo au eneo lako kwa maelezo kuhusu jinsi ya kuomba.
Usaidizi wa chakula kwa wazee
Baadhi ya majimbo hutoa usaidizi wa chakula kwa watu wenye miaka 60 au zaidi wenye kipato cha chini kupitia Programu ya Lishe ya Soko la Wakulima Wazee (SFMNP) na Programu ya Bidhaa za Chakula cha Ziada (CSFP). Programu hizi za usaidizi zinajumuisha vifurushi vya kila mwezi vya chakula bora na kuponi za chakula kwenye masoko ya wakulima. Wazee pia wanaweza kustahiki usaidizi wa chakula kutoka SNAP.
Jinsi ya kuomba: Wasiliana na programu ya chakula na lishe katika jimbo lako kwa maelezo kuhusu jinsi ya kuomba.
Milo ya bure au yenye punguzo shuleni
Shule hutoa milo ya bure au ya bei nafuu katika mwaka wa masomo na mapumziko ya kiangazi. Watoto wako wanaweza kustahiki kulingana na kipato cha kaya yako. Ukipata mafao ya SNAP au TANF, watoto wako watastahiki kiotomatiki milo ya bure shuleni.
Jinsi ya kuomba: Shule kwa kawaida hutuma maombi nyumbani mwanzoni mwa mwaka wa masomo. Unaweza pia kuiuliza ofisi ya shule yako kuhusu maombi wakati wowote katika mwaka wa masomo.
Makazi ya umma na vocha
Serikali ya Marekani inatoa makazi ya umma au ruzuku ya makazi kwa familia za kipato cha chini, wazee na watu wenye ulemavu. Makazi haya kwa kawaida hupunguziwa kodi. Unaweza pia kuomba vocha za kulipia sehemu ya kodi yako au kodi yako yote.
Jinsi ya kuomba: Wasiliana na shirika la makazi ya umma la jimbo lako kwa maelezo zaidi.
Pata habari zaidi kuhusu makazi kwa wahamiaji.
Msaada wa kulipa bili za huduma muhimu
Programu ya LIHEAP huwasaidia watu wenye kipato cha chini kulipia bili za nishati ya nyumbani, kama vile gesi na umeme.
Jinsi ya kuomba: Wasiliana na ofisi ya LIHEAP ya jimbo lako kwa maelezo zaidi.
Programu ya WAP husaidia kulipia maboresho ya nyumba yanayookoa pesa za bili za nishati.
Jinsi ya kuomba: Wasiliana na ofisi ya WAP ya jimbo lako kwa maelezo zaidi.
Lifeline huwasaidia watu wenye kipato cha chini kulipia huduma ya simu na intaneti.
Jinsi ya kuomba: Wasiliana na kampuni ya simu au mtandao ili ujisajili na huduma ya Lifeline.
Je, mnufaika wa umma ni nani?
Mnufaika wa umma (public charge) ni mtu ambaye maafisa wa uhamiaji wanaamini kuwa ataitegemea serikali kwa pesa na usaidizi. Ikiwa unachukuliwa kuwa mnufaika wa umma, huenda ukashindwa kuomba hali ya uhamiaji.
Mafao 2 tu ya umma yanahesabiwa kwa mnufaika wa umma:
- Usaidizi wa pesa taslimu za umma (ikiwemo SSI na TANF)
- Matibabu ya muda mrefu (kupitia Medicaid au programu nyingine)
Mnufaika wa umma hahusiki kwa makundi yanayostahiki huduma za ORR ikiwemo wakimbizi na watafuta hifadhi. Fahamu zaidi kuhusu mnufaika wa umma.
Mafao na huduma za ORR ni zipi?
Mafao ya muda mfupi
Mafao na huduma za ORR husaidia wakimbizi, watafuta hifadhi, na wahamiaji wengine wapya kulipia mahitaji ya msingi waingiapo Marekani. Serikali za majimbo, mashirika mahalia ya makazi mapya, na mashirika ya jumuiya hutoa huduma hizi. Pata taarifa za ORR katika lugha nyingi.
Mafao ya ORR yanapatikana kwa makundi haya:
- Wakimbizi na watafuta hifadhi
- Wasamehewa wa Afghanistan na Ukraine
- Wenye SIV wa Afghanistan na Iraq
- Wageni wa Cuba na Haiti
- Wahanga wa biashara haramu ya binadamu
- Manusura wa utesaji
- Waasia Wamarekani (Ameriasians)
Mafao ya muda mfupi
Mafao na huduma nyingi za ORR zinapatikana kwa hadi miezi 12 baada ya kufika Marekani.
Jinsi ya kuomba: Jisajili na shirika mahalia la makazi mapya ya wakimbizi mara tu unapopata hali yako. Ikiwa wewe ni mkimbizi, utaunganishwa moja kwa moja na shirika la makazi mapya. Watakusaidia kujiandikisha katika programu hizi. Zungumza na afisa wako wa ustawi ikiwa una maswali yoyote.
Mafao ya muda mfupi yanajumuisha:
Usaidizi wa pesa taslimu kwa wakimbizi (RCA)
ikiwa hustahiki SSI au TANF, unaweza kupata hadi miezi 12 ya usaidizi wa pesa taslimu. Unaweza kutumia RCA kulipia chakula, makazi na usafiri.
Unaweza pia kupata upangaji wa kujitegemea na huduma za ajira kupitia programu hii.
Mpango wa ruzuku linganifu (MG).
Unaweza kuchagua kujiandikisha katika programu ya MG badala ya RCA. MG hutoa usaidizi wa pesa taslimu, kupanga bajeti ya familia, usimamizi wa kesi, na huduma za ajira kwa hadi miezi 8 (siku 240).
Programu hii pia hutoa usaidizi wa makazi, usafiri, afya, na mafunzo ya lugha ya Kiingereza.
Usaidizi wa matibabu kwa wakimbizi (RMA)
Ukikosa ustahiki wa Medicaid, unaweza kupata hadi miezi 12 ya RMA. RMA hutoa bima ya afya ya bure au ya gharama nafuu kama Medicaid. Unaweza kuomba bima ya matibabu kupitia soko la bima ya afya baada ya RMA kuisha.
Unaweza kufanyiwa uchunguzi wa kitiba bila malipo katika idara ya afya ya eneo lako baada ya kuwasili Marekani. Itajumuisha chanjo zozote zinazohitajika. Tabibu atakupa rufaa kwenda hospitali au kwa mbobezi ikiwa utahitaji matibabu zaidi.
Huduma za muda mrefu
ORR inatoa programu za ziada zinazokusaidia baada ya mwaka wako wa kwanza hapa. Programu hizi zinalenga kukusaidia kuwa salama zaidi katika maisha yako Marekani. Huduma hizi zinapatikana kwa hadi miaka 5.
Huduma za muda mrefu zinajumuisha:
Huduma za Usaidizi kwa Wakimbizi (RSS)
Unaweza kupata huduma za usaidizi kwa hadi miaka 5 baada ya kuwasili Marekani. Hizi zinajumuisha usaidizi wa kujifunza Kiingereza, kutafuta kazi, na mafunzo. Unaweza pia kupata usaidizi kuhusu malezi ya watoto, usafiri, huduma za utafsiri na ukalimani, na usimamizi wa kesi. Unaweza pia kupata elimu ya afya na usaidizi wa afya ya akili kupitia programu hii.
Programu maalum
Baadhi ya mashirika ya makazi mapya na mashirika ya jumuiya hutoa programu maalum kama vile akiba ya kifedha, ushauri kwa vijana, huduma kwa wazee, na usaidizi wa kiufundi kwa biashara ndogo ndogo.
Kuna rasilimali za ziada kwa baadhi ya makundi husika. Fahamu zaidi kuhusu mafao ya wasamehewa wa Ukraine na wageni wa Afghanistan.
Taarifa kwenye ukurasa huu umetoka kwa USA.gov, Office of Refugee Resettlement, na vyanzo vingine vinavyoaminika. Malengo yetu ni kutoa taarifa zilizo rahisi kuelewa na zinazosasishwa mara kwa mara. Taarifa hii si ushauri wa kisheria.