Gawanya

Haki za wakimbizi na wahamiaji nchini Marekani

Kila mtu nchini Marekani ana haki za msingi bila kujali hali yake ya uhamiaji. Haki ulizo nazo hapa zinaweza kutofautiana na zile za nchi yako. Ni muhimu kujua haki zako ili uweze kujilinda wewe na familia yako.

Imesasishwa Juni 18, 2024

Basic rights

Kila mtu ana haki za msingi nchini Marekani, hata kama wewe si raia au mkazi wa kudumu. Hizi zinajumuisha haki ya kuzungumza kwa uhuru, kukutana kwa amani, kuwa salama na kutendewa kwa usawa, na kuwa na faragha.

Una haki ya kutendewa haki, bila kujali hali yako ya uhamiaji. Hii inamaanisha kuwa huwezi kubaguliwa au kuonewa kwa kuwa wewe ni mhamiaji. Ni kinyume cha sheria kwa mtu yeyote kukubagua kwa misingi ya:

  • Umri wako
  • Ulemavu wako
  • Asili yako ya utaifa
  • Mbari na rangi yako
  • Dini au imani yako
  • Utambulisho wako wa kijinsia
  • Mwelekeo wako wa kingono

Ubaguzi ni kinyume cha sheria katika nyanja zote za maisha, ikiwemo makazi, mahali pa kazi, shuleni, hospitalini na katika mashirika.

Fahamu zaidi kuhusu haki za LGBTQ+.

Haki ya makazi salama

Una haki ya kuishi katika nyumba salama na safi kiafya. Nyumba yako haipaswi kuwa na ukungu wenye sumu, uvujaji wa paa, au shambulio la wadudu.

Ikiwa una ulemavu, unaweza kuomba marekebisho katika nyumba yako ya kupanga. Watoa huduma za makazi lazima wawazingatie watu wenye ulemavu.

Wamiliki wa nyumba pia hawawezi kukataa kukupangisha au kukutoza zaidi kwa sababu ya hali yako ya uhamiaji.

Fahamu zaidi kuhusu kutafuta mahali pa kuishi.

Haki ya mahali salama pa kazi na penye haki

Una haki ya kuwa na mahali salama pa kazi na panapozingatia afya, pasipo na kemikali hatari na vifaa visivyo salama. Lazima ulipwe angalau kima cha chini cha ujira kilichowekwa na sheria za jimbo na taifa.

Mahali pako pa kazi hapapaswi kuwa na ubaguzi na unyonyaji. Mwajiri wako hapaswi kukulipa kidogo, kukunyima cheo, au kukufuta kazi kwa kuwa tu wewe ni mhamiaji. Pia una haki ya kuzungumza juu ya hali zisizo salama bila hofu ya kuadhibiwa au kupoteza kazi yako.

Wafanyakazi wasio na vibali wana haki hizi pia, ingawa inaweza kuwa changamoto kuzitumia. Unaweza kupata usaidizi kutoka kwa mashirika mahalia ya wafanyakazi na baadhi ya mashirika ya serikali bila kufichua hali yako ya uhamiaji. Makundi haya yanaweza kutoa msaada na mwongozo.

Fahamu zaidi kuhusu haki zako kazini na kupata kibali cha kufanya kazi.

Haki ya kupata elimu bure

Watoto wote wana haki ya kupata elimu ya umma bila malipo ili kupata cheti cha shule ya upili nchini Marekani. Hii inajumuisha elimu ya shule za msingi na sekondari.

Shule hazipaswi kukutendea isivyo haki kwa sababu ya rangi au kabila lako. 

Fahamu zaidi kuhusu haki na sheria za wanafunzi wahamiaji.

Haki ya huduma ya matibabu ya dharura

Una haki ya kupata huduma ya matibabu ya dharura, hata kama huna bima ya afya. Hospitali na zahanati zinatakiwa, kwa mujibu wa sheria, kutoa matibabu ya dharura kwa yeyote anayehitaji, bila kujali hali ya uhamiaji au uwezo wa kulipa.

Fahamu zaidi kuhusu kwenda kwa daktari.

Haki ya jumuiya salama

Kila mtu anastahili kuishi katika jumuiya salama. Ikiwa unahisi kutishiwa au upo katika hatari, kumbuka una haki ya kutafuta msaada. Polisi na mashirika mengine katika jumuiya yako yanaweza kukusaidia wakati wa dharura au ikiwa unakabiliwa na kitisho.

Fahamu zaidi kuhusu kukabiliana na vitisho.

Haki uwapo mikononi mwa polisi, CBP, na ICE

Una haki wakati unashughulika na maafisa wa kushurutisha sheria. Hii inajumuisha polisi, Forodha na Ulinzi wa Mipaka (CBP), na Shuruti ya Uhamiaji na Forodha (ICE).

Maafisa wanaweza kukushikilia na kukuhoji kwa muda ikiwa wanashuku ulihusika katika uhalifu. Hawawezi kukuweka kizuizini au kukutia mbaroni bila ushahidi unaoonesha kuwa umevunja sheria. Hawaruhusiwi kutumia unyanyasaji wa kimwili au matusi, mbinu za kukuogopesha au vitisho dhidi yako.

Soma zaidi kuhusu nini cha kufanya ikiwa umesimamishwa na polisi au ICE.

Haki ya kunyamaza

Ikiwa polisi au mamlaka za uhamiaji watakuuliza kuhusu hali yako ya uhamiaji au kitu kingine chochote, una haki ya kunyamaza. Hulazimiki kujibu maswali yao au kusaini nyaraka zozote bila mwanasheria kuwepo.

Unaweza tu kusema “Sitaki kujibu maswali yoyote bila wakili wangu kuwepo.” Vyombo vya sheria haviwezi kukulazimisha kujibu maswali au kukuadhibu kwa kukataa kuzungumza.

Haki ya faragha

Lazima polisi wawe na kibali kilichosainiwa na hakimu kinachotoa ruhusa ya kukupekua wewe, simu yako, gari lako au nyumba yako. Vyombo vya sheria vikija nyumbani kwako, unaweza kuzungumza bila kufungua mlango. Daima omba kuona kibali cha upekuzi. Wakiwa nacho, wanaruhusiwa kupekua eneo lililoainishwa, lakini bado una haki ya kunyamaza na kuwasiliana na wakili mara moja.

Haki ya kutendewa haki

Mamlaka za uhamiaji, kama vile ICE, zikijaribu kukuweka kizuizini au kukufukuza nchini, una haki ya kusikilizwa na hakimu wa uhamiaji. Ukiwekwa katika taratibu za kuondolewa kwa haraka, una haki ya kupewa mahojiano ya hofu sadikifu na unaweza kuomba hifadhi nchini.

Haki ya kupewa wakili

Una haki ya kupewa wakili wakati wa miingiliano yoyote na polisi. Ni muhimu kutojibu maswali au kusaini nyaraka bila kuzielewa au ni muhimu kuzungumza na wakili.

Pia una haki ya kuwakilishwa na wakili katika kesi za uhamiaji. Lazima serikali ikupatie taarifa kuhusiana na huduma za kisheria za bila malipo au za gharama nafuu.

Fahamu jinsi ya kupata msaada wa kisheria.

Haki uwapo kizuizini

Ukitiwa mbaroni au kuzuiliwa katika jela ya wahalifu, gereza, au kizuizi cha wahamiaji, una haki ya kupata msaada wa kisheria na kusikilizwa kwa haki ili kuwasilisha kesi yako. Pia una haki ya kupata mahitaji ya msingi na huduma ya matibabu.

Huwezi kuzuiliwa kwa muda usiojulikana. Kuna ukomo wa muda ambao mamlaka za uhamiaji zinaweza kukuweka kizuizini. Ikiwa upo mpakani, una haki pia ya kuomba hifadhi.

Fahamu zaidi kuhusu nini cha kutarajia ukiwa kizuizini.

Haki ya kupewa huduma ya tafsiri

Una haki ya kupewa huduma ya tafsiri bila malipo katika lugha yako kwenye huduma nyingi za serikali ya Marekani. Ikiwa huzungumzi Kiingereza kwa ufasaha, unaweza kuomba msaada. Ofisi hizi haziwezi kukataa kukupa huduma kwa sababu ya lugha yako.

Fahamu jinsi ya kupata huduma ya tafsiri bila malipo.

Haki za kupata mafao na huduma za umma

Ukihitaji usaidizi wa kulipia gharama kama vile chakula na makazi, unaweza kupata mafao ya umma kulingana na hali yako ya uhamiaji. Angalia mashirika ya huduma ya jamii ya jimbo lako kwa maelezo zaidi.

Unaweza pia kupata chakula, malazi, usafiri na usaidizi wa dharura bila malipo au kwa gharama ya chini katika jumuiya yako. Unaweza kupata aina hii ya usaidizi hata kama huna vibali vya uhamiaji.

Fahamu zaidi kuhusu mafao ya umma.

Haki ya kusafiri

Una haki ya kusafiri kwa uhuru ndani ya Marekani. Unaweza kuhama majimbo na miji na kuchagua mahali pa kuishi. Ni muhimu kubeba kitambulisho sahihi na kufuata sheria za eneo wakati wa kusafiri.

Ikiwa unapanga kusafiri nje ya nchi, unaweza kuhitaji hati ya kusafiri ili kurudi Marekani. Hii ni kulingana na hali yako ya uhamiaji. Ni muhimu kushauriana na mwakilishi wa kisheria wa uhamiaji kabla ya kusafiri ikiwa una ombi linalosubiri.

Fahamu zaidi kuhusu kupata hati ya kusafiri.

Haki ya kuomba mafao ya uhamiaji

Una haki ya kuomba programu zinazokuruhusu kuishi na kufanya kazi nchini Marekani kihalali. Ikiwa upo Marekani kihalali, unaweza kuomba Green Card ili kuishi na kufanya kazi nchini Marekani kwa kudumu na baadaye kuomba kuwa raia wa Marekani.

Pia kuna programu za masuala ya kibinadamu zinazosaidia watu kutoka nchi zenye majanga, mateso, au hali nyingine za dharura. Hii inajumuisha haki ya kutafuta hifadhi katika mpaka wa Marekani na Mexico. Aidha, Hali ya Kulindwa kwa Muda (TPS) inapatikana kwa watu kutoka nchi mahsusi. Unaweza kuomba programu hizi hata kama huna hadhi ya kisheria ya uhamiaji.

Pata maelezo zaidi kuhusu programu za masuala ya kibinadamu na TPS.

Haki ya kuungana tena na familia

Kuna programu tofauti nchini Marekani za kukusaidia kuleta familia yako ili muungane. Programu hizi zinakuwezesha kuomba visa kwa baadhi ya wanafamilia.

Fahamu zaidi kuhusu uhamiaji wa familia kwa wenye green card na kuunganishwa tena kwa familia kwa wakimbizi na wahamiaji.

Haki za wahanga wa ukatili wa majumbani

Ikiwa unafanyiwa ukatili nyumbani na mtu unayeishi naye, mwanafamilia, au mwenzi wako, una haki zako. Yeyote anayefanyiwa unyanyasaji wa nyumbani ana haki ya kusaidiwa na vyombo vya sheria na kupata makazi ya dharura, matibabu na ushauri nasaha.

Fahamu zaidi kuhusu ukatili wa majumbani na programu za kibinadamu zinazowalinda manusura kama vile U Visa na VAWA.

Haki kulingana na hali ya uhamiaji

Haki zako zinaweza kutofautiana kulingana na hali ya uhamiaji pamoja na jimbo.

Wahamiaji wasio na vibali 

Ikiwa huna vibali vya kuwepo Marekani kihalali, bado una haki zako. Una haki ya makazi salama, mahali pa kazi penye haki, elimu bure, matibabu ya dharura, kusaidiwa na vyombo vya sheria na kulindwa dhidi ya ubaguzi.

Ukiwa na DACA, unaweza kuomba leseni ya udereva, nambari ya ‘social security’ na kibali cha kufanya kazi. Kuanzia Novemba 2024, utakuwa na haki ya kuomba huduma ya afya kupitia Sheria ya Matibabu ya Gharama Nafuu (ACA).

Pata taarifa mpya kuhusu DACA na mahali pa kupata usaidizi.

Watu wasio na utaifa

Ikiwa huna utaifa, una haki za msingi, hata kama huna utaifa au uraia katika nchi yoyote ile duniani. Haki hizi zinajumuisha kupata elimu, huduma za afya, na kulindwa dhidi ya ubaguzi. Watu wasio na utaifa wanaweza pia kuomba baadhi ya mafao ya uhamiaji ili kupata hadhi ya kisheria.

Fahamu zaidi kuhusu haki za watu wasio na utaifa.

Wakimbizi na watafuta hifadhi

Serikali ya Marekani inatoa mafao na huduma za umma kwa wakimbizi na watafuta hifadhi kupitia Ofisi ya Makazi Mapya ya Wakimbizi (ORR). Zinajumuisha usaidizi wa muda wa pesa taslimu, bima ya matibabu, huduma za ajira na mafunzo ya lugha ya Kiingereza. Wakimbizi na watafuta hifadhi wanaweza pia kuomba green card baada ya mwaka 1.

Fahamu zaidi kuhusu mafao ya ORR.

Raia wa kujiandikisha

Raia wa kujiandikisha nchini Marekani wana haki sawa na wale waliozaliwa nchini. Hii inajumuisha haki ya kupiga kura, kugombea ofisi ya umma, na kuomba kazi za serikali kuu.

Haki ya kuripoti ukiukaji na unyanyasaji

Ukiamini haki zako zimekiukwa, unaweza kuripoti kwa vyombo vya sheria vya eneo lako. Polisi hawawezi kukuuliza hali yako ya uhamiaji au kukukabidhi kwa mamlaka za uhamiaji kwa sababu ya kuripoti uhalifu.

Unaweza pia kuwasiliana na rafiki unayemwamini, wakili wa uhamiaji, ofisi ya makazi mapya, au shirika la jumuiya ikiwa hutaki kuwasiliana na polisi.

FindHello app Houston search map
Find help near you

Find legal help, English classes, health clinics, housing support, and more. Search a local map and list of services for immigrants in the USA with the app FindHello.

Start your search

Taarifa kwenye ukurasa huu umetoka kwa ACLU, USCIS, na vyanzo vingine vinavyoaminika. Malengo yetu ni kutoa taarifa zilizo rahisi kuelewa na zinazosasishwa mara kwa mara. Taarifa hii si ushauri wa kisheria.

Share