Jinsi ya kupata mwanasheria wa uhamiaji bila malipo na usaidizi wa kisheria kwa gharama nafuu
Ni muhimu kupata ushauri wa kisheria unapotuma maombi yanayohusu uhamiaji au ikiwa umezuiliwa. Mashirika mengi hutoa usaidizi wa kisheria bila malipo au kwa gharama nafuu kupitia mwanasheria wa uhamiaji au mwakilishi aliyeidhinishwa. Fahamu jinsi ya kupata usaidizi wa kuaminika na jinsi unavyoweza kujiwakilisha mwenyewe.
Msaada wa kisheria ni nini?
Msaada wa kisheria ni ushauri kuhusu sheria na uwakilishi mahakamani. Wanasheria, mawakili, na wawakilishi walioidhinishwa wanaweza kutoa usaidizi wa kisheria. Nchini Marekani, maneno mwanasheria na wakili mara nyingi hutumiwa kwa njia sawa.
Wanasheria wamebobea katika maeneo tofauti kama vile majeraha binafsi, sheria ya jinai, mali isiyohamishika na masuala ya familia. Ukurasa huu unaangazia usaidizi wa uhamiaji lakini pia unatoa rasilimali kadhaa kwa mahitaji mengine ya kisheria.
Pro bono ni kazi inayofanywa na mwanasheria bila malipo. Ni msaada wa kisheria unaotolewa kwa watu wenye kipato cha chini. |
Je, kwa nini ni muhimu kupata usaidizi wa kisheria?
Huhitajiki kuwa na mwanasheria lakini mchakato wa uhamiaji nchini Marekani ni mgumu. Mwansheria wa uhamiaji anaweza kukusaidia kuwasilisha fomu za uhamiaji na kukutetea mahakamani. Utafanikiwa zaidi ukiwa na usaidizi wa kisheria.
Mwanasheria wa uhamiaji anaweza kukusaidia kupata mafao ya uhamiaji kama vile green card, hifadhi, au uraia. Anaweza kukusaidia:
- Kuperuzi chaguzi zako na hatua zinazofuata
- Kuelewa maswali yanayohusiana na maombi yako na fomu
- Kuepuka makosa kwenye maombi yako ambayo yanaweza kufanya suala lako likataliwe
- Kuwasilisha maombi yako na hati zinazounga mkono maombi hayo
- Kujiandaa kwa mahojiano yoyote na kupata mkalimani
- Kupata taarifa mpya na maamuzi kuhusu suala lako
- Kuboresha uwezekano wako wa kufanikiwa suala lako
- Kukata rufani dhidi ya uamuzi
Je, wakati gani napaswa kupata usaidizi wa kisheria?
Unaweza kupata usaidizi wa kisheria wakati wowote. Ikiwa unatafuta usaidizi wa kubadilisha hali yako ya uhamiaji, ni vyema kuwa na mtu wa kukagua maombi yako kabla ya kuyatuma. Si kila wakati kuna wanasheria wa kutosha wa masuala ya uhamiaji kwa kila suala husika. Wakati mwingine inaweza kuchukua muda kupata usaidizi sahihi.
Ni muhimu kupata usaidizi wa kisheria ikiwa una kesi ya kuondolewa katika mahakama ya uhamiaji. Serikali haitoi ushauri wa bure wa kisheria kwa watu walio katika kesi za uhamiaji. Utapewa orodha ya wanasheria wa bila malipo au wa gharama nafuu unaoweza kuwasiliana nao.
Kuna hali nyingine, zaidi ya uhamiaji, ambapo kuwa na mwanasheria ni muhimu. Hii inaweza kujumuisha masuala ya sheria ya familia, masuala ya ajira au makazi, kesi za jinai, kuelewa hati za kisheria na mikataba, matatizo ya kupata mafao ya umma, madai ya majeraha binafsi na kuanzisha biashara.
Je, nani anaweza kunipa usaidizi wa kisheria?
Wataalamu wafuatao wanaweza kutoa ushauri na huduma za kisheria katika masuala ya uhamiaji na uraia:
- Mwanasheria au wakili wa uhamiaji: aliyepewa leseni na chama cha wanasheria wa jimbo kutoa usaidizi wa kisheria. Wakili amehitimu shule ya sheria na ana digrii ya Juris Doctor (J.D).
- Mwakilishi aliyeidhinishwa na DOJ: mtu binafsi au shirika lisilo la kutengeneza faida lenye ujuzi wa kutoa huduma za uhamiaji na lililoidhinishwa na Idara ya Haki (DOJ).
Wakili wa masuala ya uhamiaji na mwakilishi aliyeidhinishwa kikamilifu wote wanaweza kukuwakilisha mbele ya DHS, USCIS, EOIR (mahakama ya uhamiaji), na BIA (rufani za uhamiaji). Mwakilishi aliyeidhinishwa kwa sehemu anaweza kukuwakilisha mbele ya USCIS tu.
Je, nawezaje kupata usaidizi wa kisheria wa kuaminika?
Ikiwa unatafuta usaidizi kuhusu kesi ya uhamiaji, hakikisha unazungumza na mwanasheria mwenye uzoefu katika sheria za uhamiaji. Mwanasheria ambaye si mtaalamu wa sheria za uhamiaji anaweza asikupe ushauri sahihi.
Pia, tambua kwamba baadhi ya kampuni hujifanya kutoa huduma za kisheria za uhakika ili kupata pesa. Kuna baadhi ya mambo rahisi unaweza kufanya ili kujilinda.
Kwa mwanasheria wa masuala ya uhamiaji:
- Omba kuona nakala ya leseni yake
- Angalia kama yupo katika hali nzuri na Chama cha Wanasheria wa Jimbo na Chama cha Wanasheria wa Masuala ya Uhamiaji wa Marekani (AILA)
Kwa mwakilishi aliyeidhinishwa:
- Omba kuona uthibitisho wa kibali cha idhinisho
- Angalia kama yupo kwenye orodha ya DOJ
Vidokezo vya ziada:
- Tafiti chaguzi zaidi na wasiliana na zaidi ya mwanasheria mmoja
- Uliza kama anatoa mashauriano bila malipo
- Uliza maswali kuhusu aina ya kesi wanazozishughulikia na huduma wanazotoa
- Uliza ratiba kamili ya ada na malipo yanayohitajika kabla ya kuanza
- Chukua muda kupitia mkataba au makubaliano yoyote kabla ya kusaini
- Uliza kama ana hati punguzo la ada ili kupunguza gharama
Hati punguzo la ada inamaanisha gharama ya huduma ya mwanasheria inategema na kipato chako. Kadri unavyolipwa kidogo zaidi kwenye kazi yako, ndivyo utakavyolipa kidogo zaidi kwa usaidizi wa kisheria. |
Epuka ulaghai na kuwa mwangalifu na mtu yeyote ambaye:
- Anakuwa wa kwanza kukutafuta wewe
- Anaahidi mambo ambayo si rahisi kuamini ni ya kweli
- Anatoa uhakikisho au anakuahidi mafao
- Anatoa huduma za kisheria kwa sharti la kutaka kitu fulani kutoka kwako
- Anakataa kuunda mkataba au makubaliano
- Anajaribu kushikilia hati zako halisi
- Anatoza gharama kwa fomu tupu za uhamiaji
Elewa jinsi ya kujilinda dhidi ya wanasheria feki (notarios) na tovuti bandia. Fahamu nini cha kufanya ikiwa umekuwa mhanga wa ulaghai.
Je, wapi naweza kupata usaidizi wa kisheria bila malipo au kwa gharama nafuu?
Unaweza kupata wanasheria wa uhamiaji na wawakilishi walioidhinishwa na DOJ wanaotoa usaidizi bila malipo au kwa gharama nafuu kupitia mashirika yasiyo ya kutengeneza faida na programu za kisheria za uhamiaji. Unaweza pia kuwaomba watu unaowaamini wakupe mapendekezo.
Rasilimali | Msaada |
---|---|
Directory of immigration lawyers. Hawa wanaweza kutoza ada tofauti kulingana na kesi yako. Wasiliana nao moja kwa moja ili kujua kama wanatoa ushauri bila malipo | |
Kuwa mwanachama wa ASAP hukupa ufikio wa bila malipo kwa mawakili wataalam wa uhamiaji, watafuta hifadhi wengine, na rasilimali muhimu. | |
Unganishwa na usaidizi wa kisheria mtandaoni bila malipo, ili kusaidia mchakato wako wa uraia | |
Inatoa orodha ya watoa huduma za kisheria wa pro bono kwa kila jimbo | |
Orodha ya mtandaoni ya mashirika yasiyo ya kutengeneza faida yanayotoa huduma za kisheria za uhamiaji bila malipo au kwa gharama nafuu. Tafuta usaidizi wa kisheria kulingana na jimbo, msimbo wa posta, kituo cha kizuizini, eneo la uhamiaji na aina za huduma | |
Inatoa rasilimali za kisheria kwa LGBTQ+ na/au jumuiya za wahamiaji wenye VVU, ikiwemo taarifa kuhusu hifadhi na kizuizini. | |
Inatoa usaidizi wa kisheria kwa wageni kutoka Afghanistan | |
Nambari ya simu kwa wakimbizi na watafuta hifadhi ili kuzungumza na mtu kwa usaidizi. Piga 202-461-2356 au #566 kupitia simu ya kituo cha kizuizini | |
Tafuta mashirika na nambari za usaidizi ikiwa wewe au mpendwa wako umezuiliwa au ametenganishwa na familia |
Ikiwa unatafuta usaidizi wa kisheria nje ya Marekani, pata maelezo kwenye ukurasa wetu wa usaidizi wa kimataifa.
Find legal help, English classes, health clinics, housing support, and more. Search a local map and list of services for immigrants in the USA with the app FindHello.
Je, nawezaje kupata usaidizi ikiwa najiwakilisha mwenyewe?
Ikiwa unajiwakilisha mwenyewe katika mahakama ya uhamiaji, zipo rasilimali za kukusaidia.
- Uliza chama cha wanasheria wa eneo lako, chuo kikuu, au wakala wa makazi mapya kuhusu warsha na programu za kisheria bila malipo.
- ASAP huorodhesha mashirika yanayotoa usaidizi wa kisheria kwa watafuta hifadhi ambao wanajiwakilisha wenyewe.
- The Florence Project ina rasilimali za kujisaidia kwa wahamiaji walio kizuizini.
- DOJ inatoa nyenzo za kujisaidia.
Pro se ni neno linalotumiwa wakati mtu anajiwakilisha mwenyewe mahakamani na hana wakili. Ni neno la Kilatini linalomaanisha “kwa niaba ya mtu mwenyewe.” |
Je, wapi naweza kupata usaidizi wa kisheria kwa mahitaji mengine?
Kuna usaidizi wa kisheria unaopatikana katika maeneo nje ya uhamiaji. Ofisi nyingi za usaidizi wa kisheria hutoa msaada bila malipo au kwa gharama nafuu kwa watu wenye matatizo ya masuala ya wateja, ukatili wa familia na majumbani, makazi, mafao ya umma, na ajira.
- Chama cha Wanasheria wa Marekani hutoa rasilimali za kutafuta usaidizi wa kisheria bila malipo.
- LawHelp.org ina miongozo ya taarifa za kisheria na orodha ya programu za msaada wa kisheria bila malipo.
- Law Help Interactive ina miongozo ya bure ya jinsi ya kujaza fomu za kisheria.
Je, haki zangu ni zipi?
Kila mtu ana haki ya kupata usaidizi wa kisheria. Hutapewa wakili wa bure katika mahakama ya uhamiaji. Ni jukumu lako kupata usaidizi wa kisheria. Utapewa orodha ya wanaotoa huduma za kisheria bila malipo au kwa gharama nafuu katika mahakama ya uhamiaji.
Unaweza kuwasilisha malalamiko dhidi ya wakili wako kwa chama chake cha jimbo au kwa Ofisi Kuu ya Ukaguzi wa Masuala ya Uhamiaji. Unaweza kubadilisha mawakili ikiwa wakili wako haelezei machaguo yako katika kesi ya uhamiaji au hawasilishi hati/nyaraka zinazohitajika. Wewe au wakili wako mpya mnaweza kuomba nakala ya faili la kesi yako.
Unapaswa kuripoti ulaghai wa uhamiaji kwa USCIS, Ofisi Kuu ya Ukaguzi wa Masuala ya Uhamiaji, au Tume ya Biashara ya Serikali Kuu.
Taarifa kwenye ukurasa huu umetoka kwa LawHelp.org, the National Immigrant Justice Center, the Department of Justice, UNHCR, na vyanzo vingine vinavyoaminika. Malengo yetu ni kutoa taarifa zilizo rahisi kuelewa na zinazosasishwa mara kwa mara. Taarifa hii si ushauri wa kisheria.