Haki za wakimbizi na wahamiaji nchini Marekani

Imerekebishwa Machi 18, 2025
Ukurasa huu ulitafsiriwa kitaalamu na mwanadamu. Jifunze zaidi
Kila mtu nchini Marekani ana haki za msingi bila kujali hadhi zao za uhamiaji. Haki ulizo nazo hapa zinaweza kuwa tofauti na zile za nchini kwako. Ni muhimu kujua haki zako ili uweze kujilinda wewe mwenyewe na familia yako.

Jua haki zako za msingi

Kila mtu ana haki za msingi nchini Marekani, hata kama wewe si raia au mkazi wa kudumu. Haki hizo ni pamoja na haki ya kuzungumza kwa uhuru, kukutana kwa amani, kuwa salama na kutibiwa kwa usawa, na kuwa na faragha.

Ubaguzi ni kinyume cha sheria katika nyanja zote za maisha, ikiwa ni pamoja na makazi, mahali pa kazi, shule, hospitali na biashara. Hakuna mtu anayepaswa kukutendea vibaya kwa sababu yako:

  • Umri
  • Ulemavu
  • Asili ya taifa
  • Jamii na rangi
  • Dini au imani
  • Utambulisho wa kijinsia
  • Mwelekeo wa kingono

Hata hivyo, mabadiliko ya sera ya hivi majuzi na ongezeko la utekelezaji wa sheria za uhamiaji hufanya iwe vigumu kwa baadhi ya wahamiaji, hasa wale wasio na hadhi ya kisheria, kutumia haki zao.

Haki ya polisi, CBP, na ICE

Una haki unaposhughulika na maafisa wa utekelezaji wa sheria. Hii ni pamoja na polisi, Customs and Border Protection (CBP), na Immigration and Customs Enforcement (ICE).

Maafisa wanaweza kukushikilia na kukuhoji kwa ufupi ikiwa wanashuku kuwa ulihusika katika uhalifu. Hawawezi kukuzuia au kukukamata bila ushahidi unaoonyesha kuwa umevunja sheria. Hawaruhusiwi kutumia unyanyasaji wa kimwili au matusi, mbinu za vitisho au vitisho dhidi yako. Jifunze zaidi kuhusu nini cha kufanya ikiwa utasimamishwa au kukamatwa na polisi.

CBP inafanya kazi mpakani na kwenye viwanja vya ndege, huku ICE inaweza kufanya uvamizi majumbani au sehemu za kazi. Tazama mwongozo wetu wa jinsi ya kujiandaa kwa ICE ili kujifunza kuhusu haki zako, nini cha kutarajia, na jinsi ya kuunda mpango wa usalama.

Haki ya kukaa kimya

Ikiwa polisi au mamlaka za uhamiaji wanakuuliza kuhusu hadhi yako ya au kitu kingine chochote, una haki ya kukaa kimya. Sio lazima ujibu maswali yao au kusaini hati zozote bila uwepo wa wakili.

Unaweza kusema tu "Sitaki kujibu maswali yoyote bila mwanasheria wangu kuwepo." Watekelezaji wa sheria hawawezi kukukulazimisha kujibu maswali au kukuadhibu kwa kukataa kuzungumza.

Haki ya faragha

Polisi lazima wawe na kibali kilichosainiwa na hakimu anayetoa ruhusa ya kukutafuta wewe, simu yako, gari lako, au nyumba yako. Ikiwa watekelezaji wa sheria wanakuja nyumbani kwako, unaweza kuzungumza kupitia mlangoni. Omba kuona vibali vyao kila wakati. Wakifanya hivyo, wanaruhusiwa kulipekua eneo mahsusi, lakini bado una haki ya kukaa kimya na kuwasiliana na mwanasheria mara moja.

Haki ya kutendewa haki

Ikiwa mamlaka za uhamiaji, kama vile ICE, wanajaribu kukuweka kizuizini au kukufukuza nchini, una haki ya kusikilizwa mbele ya hakimu wa uhamiaji. Ikiwa uko katika kesi za haraka za kuondolewa, una haki ya mahojiano ya hofu ya vitisho na unaweza kuomba hifadhi.

Haki ya kuwa na wakili

Una haki ya kuwa na wakili wakati wa mwingiliano wowote na polisi. Ni muhimu kutojibu maswali au kusaini hati bila kuzielewa au kuzungumza na wakili.

Pia, una haki ya kuwakilishwa na wakili katika kesi za uhamiaji. Serikali inapaswa kukupa taarifa kuhusu huduma za kisheria za bila malipo au za gharama nafuu.

Pata maelezo ya jinsi ya kupata msaada wa kisheria.

Haki katika kizuizi

Kama umekamatwa au umezuiliwa katika gereza la jinai, gerezani, au katika kizuizi cha uhamiaji, una haki ya msaada wa kisheria na kusikilizwa kwa haki ili kuwasilisha kesi yako. Pia, una haki ya mahitaji ya msingi na huduma ya matibabu.

Huwezi kuzuiliwa kwa muda usiojulikana. Kuna mipaka ya muda ambao mamlaka za uhamiaji zinaweza kukuweka kizuizini. Ikiwa uko mpakani, pia una haki ya kuomba hifadhi.

Pata maelezo zaidi kuhusu kitu cha kukitarajia unapokuwa kizuizini.

Haki za ukatili wa majumbani victims

Ikiwa unakabiliwa na unyanyasaji nyumbani kutoka kwa mtu unayeishi naye, mwanafamilia, au mwenzi, una haki. Mtu yeyote anayepitia ukatili wa majumbani ana haki ya kupata msaada kutoka kwa watakelezaji wa sheria na kupata makazi ya dharura, huduma ya matibabu, na ushauri.

Pata maelezo zaidi kuhusu ukatili wa majumbani na mipango ya kibinadamu ambayo inawalinda manusura kama vile U Visa na VAWA.

Haki ya kupata makazi salama

Una haki ya kuishi katika nyumba salama na nzuri. Nyumba yako haipaswi kuwa mambo kama vile kuvu za sumu, uvujaji wa paa, au uvamizi wa wadudu.

Ikiwa una ulemavu, unaweza kuomba mabadiliko muhimu katika nyumba yako uliyopanga. Watoa huduma wa nyumba lazima wakubali watu wenye ulemavu.

Pia, wamiliki wa nyumba hawawezi kukataa kukupangisha au kukulipisha zaidi kwa sababu ya hadhi yako ya uhamiaji.

Pata maelezo zaidi kuhusu kupata mahali pa kuishi.

Haki ya kuwa na mahali pa kazi salama na pazuri

Una haki ya kuwa na mahali pa kazi salama na pazuri, pasipo na kemikali za hatari na vifaa visivyo salama. Lazima ulipwe angalau kima cha chini cha mshahara kilichowekwa na sheria za jimbo na taifa.

Mahali pako pa kazi panapaswa kutokuwa na ubaguzi na unyanyasaji. Mwajiri wako hawezi kukulipa kidogo, kukataa kukupandisha cheo, au kukufukuza kazi kwa sababu tu wewe ni mhamiaji. Pia, una haki ya kuzungumza kuhusu mazingira yasiyo salama bila hofu ya adhabu au kupoteza kazi yako.

Pia, wafanyakazi wasio na hati wana haki hizi, ingawa wanaweza kukabiliwa na changamoto za kuzitumia. Unaweza kupata msaada kutoka kwenye mashirika ya wafanyikazi ya eneo lako na baadhi ya mashirika ya serikali bila kutaja hadhi yako ya uhamiaji. Vikundi hivi vinaweza kutoa msaada na mwongozo.

Pata maelezo zaidi kuhusu haki zako kazini na kupata kibali cha kazi.

Haki ya kupata elimu ya bure

Watoto wote wana haki ya kupata elimu ya serikali ya bila malipo ili kupata diploma ya shule ya sekondari nchini Marekani. Hii inajumuisha elimu ya msingi na sekondari.

Shule haziwezi kukutendea isivyo haki kwa sababu ya rangi au kabila lako.

Fahamu zaidi kuhusu haki na sheria za mwanafunzi muhamiaji.

Haki ya huduma ya matibabu ya dharura

Una haki ya kupata huduma ya matibabu ya dharura, hata kama huna bima ya afya. Hospitali na zahanati zinahitajika kisheria kutoa matibabu ya dharura kwa yeyote anayehitaji, bila kujali hali ya uhamiaji au uwezo wa kulipa. Sio lazima kushiriki hali yako ya uhamiaji hata mtu akiuliza. Watoa huduma za afya hawawezi kukataa matibabu ikiwa utachagua kutoshiriki.

Pata maelezo zaidi kuhusu kwenda kwa daktari.

Haki ya kuwa na jamii salama

Kila mtu anastahili kuishi katika jamii salama. Ikiwa unahisi kutishiwa au uko katika hatari, kumbuka una haki ya kutafuta msaada. Polisi na mashirika mengine katika jamii yako yanaweza kukusaidia wakati wa dharura au ikiwa unakabiliwa na tishio.

Pata maelezo zaidi kuhusu kushughulikia vitisho.

Haki ya kupata msaada wa tafsiri

Una haki ya kupata msaada wa bure wa tafsiri katika lugha yako kwa huduma nyingi za serikali ya Marekani. Ikiwa huzungumzi Kiingereza kwa ufasaha, unaweza kuomba msaada. Ofisi hizi haziwezi kukataa kukupa huduma kwa sababu ya lugha yako.

Pata maelezo ya jinsi ya kupata msaada wa bure wa tafsiri.

Haki za kupata ruzuku na huduma za serikali

Ikiwa unahitaji msaada kulipia gharama kama vile chakula na makazi, unaweza kupata ruzuku za serikali kulingana na hadhi yako ya uhamiaji. Angalia mashirika yako ya huduma za kijamii ya jimbo kwa taarifa zaidi.

Pia, unaweza kupata chakula, makazi, usafiri, na msaada wa dharura wa bila malipo au wa gharama nafuu katika jamii yako. Unaweza kupata aina hii ya msaada hata kama huna hati.

Pata maelezo zaidi kuhusu ruzuku za serikali.

Haki ya kusafiri

Una haki ya kusafiri kwa uhuru ndani ya Marekani. Unaweza kwenda katika majimbo na miji mingine na kuchagua mahali pa kuishi. Ni muhimu kubeba kitambulisho sahihi na kufuata sheria za eneo husika unapokuwa safarini.

Kama unapanga kusafiri nje ya nchi, unaweza kuhitaji hati ya kusafiri kurudi Marekani. Hii inategemea hadhi yako ya uhamiaji. Ni muhimu kuwasiliana na mwakilishi wa kisheria wa uhamiaji kabla ya kusafiri ikiwa una ombi linalosubiri uamuzi.

Pata maelezo zaidi kuhusu kupata hati ya kusafiria.

Haki ya kuomba ruzuku ya uhamiaji

Una haki ya kuomba mipango inayokuwezesha kuishi na kufanya kazi nchini Marekani kihalali. Ikiwa uko Marekani kihalali, unaweza kuomba Green Card ili kuishi na kufanya kazi nchini Marekani kudumu na baadaye kuomba kuwa raia wa Marekani.

Pia, kuna mipango ya kibinadamu ambayo huwasaidia watu kutoka nchi zinazopata maafa, mateso, au hali zingine za dharura. Hii ni pamoja na haki ya kutafuta hifadhi kwenye mpaka wa Marekani na Mexico. Aidha, Hali ya Ulinzi wa Muda (TPS) inapatikana kwa watu kutoka nchi mahsusi. Unaweza kuomba mipango hii hata kama huna hadhi halali ya uhamiaji.

Pata maelezo zaidi kuhusu kuomba hifadhi na TPS.

Haki ya kuungana tena na familia

Kuna mipango mbalimbali nchini Marekani ya kukusaidia kuileta familia yako hapa kujiunga nawe. Mipango hii hukuwezesha kuomba visa kwa wanafamilia fulani.

Pata maelezo zaidi kuhusu uhamiaji wa familia kwa wamiliki wa Green Card na kuunganishwa familia za wakimbizi na waomba hifadhi.

Ramani ya utafutaji wa Houston wa programu ya FindHello
Kupata msaada ulio karibu na wewe

Pata msaada wa kisheria, madarasa ya Kiingereza, kliniki za afya, msaada wa nyumba, na zaidi. Tafuta ramani ya eneo lako na orodha ya huduma kwa wahamiaji nchini Marekani na programu ya FindHello.

Anza utafutaji wako

Taarifa kwenye ukurasa huu inatoka ACLU, USCIS, na vyanzo vingine vinavyoaminika. Tunakusudia kutoa taarifa rahisi kueleweka ambazo zinarekebishwa mara kwa mara. Taarifa hii sio ushauri wa kisheria.