Utapeli wa uhamiaji ni nini?
Utapeli au udanganyifu ni pale ambapo mtu anapodanganya ili kuiba taarifa zako binafsi au pesa zako. Ni kinyume cha sheria lakini ni jambo la kawaida. Unaweza kukutana na utapeli wa uhamiaji unapowasilisha maombi ya huduma za uhamiaji. Taarifa binafsi zinatumika kuiba utambulisho wako na yanaweza kujumuisha:
- jina na anwani yako
- akaunti ya benki na namba ya kadi ya mkopo
- namba ya hifadhi ya jamii
- nambari za bima ya afya
Kama mtu anaomba taarifa hizi, kuwa makini. Toa tu taarifa hizi kwa mtu unayemwamini. Usitoe taarifa hizi kwa mtu yeyote anayeomba kupitia simu, barua pepe, ujumbe mfupi, au mitandao ya kijamii.
Ulaghai wa ada ya uhamiaji
Utapeli wa kuomba malipo kwa ajili ya ada za uhamiaji ni kawaida. Ada za uhamiaji na maombi yanashughulikiwa kupitia U.S. Citizenship and Immigration Services (USCIS), U.S. Department of State (DOS) na Department of Justice’s (DOJ) Executive Office for Immigration Review (EOIR).
USCIS itakubali tu malipo mtandaoni kupitia akaunti yako ya myUSCIS au kwa njia ya posta kupitia maeneo yao rasmi ya lockbox. Unapokamilisha maombi mtandaoni, utaelekezwa kulipa ada kwenye pay.gov.
USCIS kamwe haitaomba:
- Malipo kupitia simu au barua pepe
- Malipo kupitia huduma kama vile Western Union, MoneyGram, PayPal, Venmo, Cash App, Zelle, kadi za zawadi au sarafu za mtandaoni
- Kutuma pesa kwa mtu au kumlipa mtu binafsi
Fomu zote za uhamiaji za USCIS na EOIR zinapatikana bila malipo kwenye USCIS.gov na justice.gov. Hakuna mtu anayepaswa kukulipisha ili kupata fomu. |
Ulaghai wa uhamiaji wa kisheria
Kuwa makini unapotafuta msaada wa kisheria. Ni mawakili tu na wawakilishi walioidhinishwa na DOJ ndiyo wanaoruhusiwa kutoa ushauri wa kisheria.
Notarios Publicos
Katika nchi nyingi za Amerika ya Kusini na Ulaya, notario publicos (wathibitishaji wa serikali) ni mawakili wenye leseni walioidhinishwa kutoa ushauri wa kisheria.
Nchini Marekani, wathibitishaji husimamia viapo na kushuhudia kusainiwa kwa nyaraka muhimu. Nchini Marekani wathibitishaji rasmi hawana mafunzo au hawajaidhinishwa kutoa huduma zozote za kisheria. Nchini Marekani wathibitishaji wanaojaribu kukulaghai wanaweza:
- Hujifanya wanatoa huduma za kisheria
- Wanasaidaia kuwasilisha maombi ya USCIS bila utaalam unaohitajika
- Huhifadhi hati zako halisi
- Kukuomba usaini fomu tupu zenye taarifa za uongo
- Kutoa ushauri wa uongo wa kisheria unaosababisha matatizo katika kesi yako ya uhamiaji
Kidokezo:
- Hakikisha unapata ushauri wa kisheria kutoka kwa wakili wa uhamiaji mwenye leseni au mwakilishi wa kisheria aliyeidhinishwa. Jifunze jinsi ya kupata watoa huduma wa kisheria unaoweza kuwaamini.
Tovuti za utapeli wa uhamiaji
Tovuti ya utapeli wa uhamiaji inaweza kujifanya kutoa maelekezo na msaada wa kuwasilisha maombi ya USCIS. Tovuti za utapeli wakati mwingine hujaribu kuonekana kama tovuti rasmi na zinaweza kutumia mtindo unaofana au muhuri rasmi. Wanaweza kuwa na makosa ya kipekee ya kuandika.
Vidokezo:
- Hakikisha tovuti iko salama kwa kutumia anwani ya “https” na alama ya kufuli (🔒)
- Tovuti rasmi za serikali zinaishia kwa .gov
- Tumia tovuti rasmi: USCIS.gov, DHS.gov, justice.gov
- Pakua fomu za bure za serikali kutoka kwenye tovuti rasmi
- Usitumie tovuti zinazojaribu kuwa na anwani inayofanana kama USCIS-online.org
- Boresha mifumo ya simu na kompyuta zako pindi matoleo mapya yametoka
- Tumia manenosiri yenye nguvu na uthibitishaji wa hatua mbili
Barua pepe za utapeli wa uhamiaji
Barua pepe za utapeli ni za kawaida sana. Barua pepe nyingi za utapeli zina faili au viungo vinavyopakua programu hasidi kwenye kifaa chako unapovibofya. Wanaweza kuomba taarifa binafsi, kama vile namba za akaunti, au kuomba malipo.
Barua pepe zinazotiliwa shaka zinaweza kuwa na:
- Makosa yasiyo ya kawaida, kama vile katika jina lako
- Herufi za ajabu na fonti zinazobadilika
- Viungo kwenda kwenye tovuti bandia za serikali
Vidokezo:
- Usifungue barua pepe zinazotiliwa shaka
- Kuwa mwangalifu unapofungua barua pepe kutoka kwa mtu usiyemfahamu
- Barua pepe zote kutoka USCIS au serikali ya Marekani zitamalizika wakati wote kwa .gov
- Usibonyeze viungo vyovyote
- Google au andika anwani ya tovuti badala ya kubofya viungo
- Usifanye malipo kupitia barua pepe
- Usijibu barua pepe zinazotiliwa shaka
- Kuwa makini na barua pepe yoyote inayodai kuwa na uamuzi wa USCIS
- Nenda kwenye myUSCIS ili uhakikishe kuwa unapata taarifa sahihi (taarifa zote muhimu zitakuwepo)
[email protected] ni barua pepe ya ulaghai. Usifungue barua pepe kutoka kwa anwani hii au bonyeza viungo vyake chochote. |
Utapeli wa uhamiaji na ujumbe
Watu wengi hupigiwa simu na kutumiwa jumbe za ulaghai. Mara nyingi walaghai hubadilisha kitambulisho cha mpiga simu ili kuendana na msimbo wa eneo lako ili uweze kupokea.
Mpiga simu ya utapeli anaweza:
- kujifanya kuwa afisa wa uhamiaji
- kuomba taarifa binafsi au malipo
- kusema taarifa zako si sahihi au unadaiwa ada na kutishia kukuripoti
Vidokezo:
- USCIS haiombi taarifa binafsi au malipo kwa njia ya simu
- Wasiliana na USCIS au EOIR ikiwa huna uhakika kama simu ni halisi
- Tafuta mawasiliano ya shirika kwenye tovuti rasmi
- Kata simu zinazotiliwa shaka na usijaribu kuzipigia
- Zuia simu na jumbe za maandishi zisizohitajika
- Wasiliana na wakili wa uhamiaji au mwakilishi ikiwa una maswali
Pia, matapeli wanaweza kuwasiliana nawe kwenye mitandao ya kijamii ili kukupa msaada wa ombi la uhamiaji, kama vile msamaha wa kibinadamu. USCIS haitawasiliana nawe kupitia Facebook, Twitter, LinkedIn, WhatsApp, au majukwaa mengine ya mtandaoni.
Utapeli wa uhamiaji wa kawaida
Hapa kuna orodha ya utapeli maalum wa uhamiaji ambao mamlaka zinatoa kwa umma. Soma maagizo kwenye maombi ili kujua mahali pa kuyatuma na kujua ikiwa umeidhinishwa.
Utapeli wa utekelezaji wa sheria za uhamiaji
Matapeli wanaweza kujifanya maafisa wa ICE ili kukulenga. Wanaweza kupiga simu, kutuma ujumbe mfupi wa maandishi, kutuma barua pepe, au kukutumia ujumbe kwenye mitandao ya kijamii wakiomba taarifa binafsi au pesa ili kuepuka kufukuzwa. ICE na polisi wa eneo lako hawapaswi kuwasiliana na watu binafsi ili kuwaonya kuhusu kufukuzwa nchini.
Ikiwa mtu anakuzuia akidai kuwa ni afisa wa uhamiaji, omba uone beji yake na ujue ni idara gani anayofanyia kazi. Usisaini makaratasi yoyote bila mwanasheria. Jitayarishe kwa uvamizi wa ICE.
Wizi wa taarifa binafsi za Afghanstani
Wezi wa taarifa binafsi za Afghanstani wanaweza kukuomba utoe taarifa binafsi ili kukusaidia kupata ruzuku za uhamiaji. USCIS kwa kawaida haitumi barua pepe kukujulisha kwamba umeidhinishwa kwenye ruzuku fulani ya uhamiaji.
Utapeli wa kuharakisha mchakato
Utapeli wa kuharakisha mchakato unaweza kukuahidi kupata haraka visa, Green Card, au kibali cha kufanya kazi ikiwa utalipa ada. Hii wanaiita "kuruka mstari." Wanaweza pia kusema wana watu wa kuwasiliana nao serikalini ili kuharakisha suala lako. Hakuna mtu anayeweza kuharakisha huduma zaidi ya muda wa kawaida ushughulikiaji wa uhamiaji.
Barua pepe za utapeli wa Fomu I-9
Utapeli wa barua pepe wa Fomu ya I-9 unaweza kuwaomba waajiri taarifa za Fomu ya I-9, wakijifanya kuwa maafisa wa USCIS. Waajiri hawapaswi kuwasilisha Fomu I-9 kwa USCIS.
Utapeli wa msamaha wa kibinadamu
Utapeli wa msamaha wa kibinadamu unaweza kulenga wahamiaji na wafadhili ili kuwatumia vibaya. Matapeli wanaweza kuwasiliana na wewe mtandaoni au kupitia mitandao ya kijamii na kujitolea kuwa wasaidizi wako kwa malipo au kwa kutoa taarifa binafsi kama namba ya pasipoti yako au tarehe ya kuzaliwa.
Wafadhili wanawajibika kutoa msaada wa kifedha kwa wanufaika kwa muda wa hadi miaka 2. Wanufaika hawapaswi kulipa au kufanya kazi kwa mfadhili wao. Wadhamini na wanufaika hawapaswi kulipa ada ya kuwasilisha maombi.
Utapeli wa usafirishaji haramu wa binadamu
Utapeli wa usafirishaji haramu wa binadamu unaweza kutokana na utapeli wa ajira unaohusisha ofa za kazi zinazotiliwa shaka zinazotumwa nje ya nchi au kupitia barua pepe. Usafirishaji haramu wa binadamu unajumuisha hali ambapo unalazimishwa kufanya kazi na hauwezi kuondoka kwa sababu ya vitisho, madeni, na hadhi ya uhamiaji. Usilipe mtu yeyote anayekuahidi kazi au cheti.
Tafuta vidokezo vya usalama ili kuepuka usafirishaji haramu wa binadamu.
Utapeli wa wakimbizi
Matapeli wa wakimbizi wanakwambia kuwa wanastahili ruzuku maalum ya serikali na wanakuomba ulipe kwanza au utoe taarifa zako za benki. Utapeli huu unaomba pesa ili kukusaidia na hadhi yako ya uhamiaji.
Utapeli wa TPS
Matapeli wa TPS mara nyingi hutoa taarifa za uwongo kuhusu kusajiliwa tena kwa TPS. Udanganyifu huu unaweza kukuomba uwasilishe fomu na malipo ili kuhuwisha TPS yako. Kuhuwisha ni bure. Usilipe wala usiwasilishe fomu yoyote hadi USCIS itakaporekebisha taarifa rasmi za TPS mtandaoni.
Utapeli wa bahati nasibu ya Visa
Utapeli wa bahati nasibu ya Visa unaweza kusema umechaguliwa kwenye mpango wa Visa ya Anuai (DV). Idara ya Jimbo haitakutumia barua pepe kuhusu kuchaguliwa kwenye bahati nasibu ya visa. Bahati nasibu ya Visa ni bure. Huna haja ya kulipa ada ili kutuma ombi.
Jinsi ya kuripoti utapeli na udanganyifu wa uhamiaji
Kuripoti kuhusu utapeli wa uhamiaji kunaweza kukusaidia. Pia, kunaweza kusaidia kuhakikisha kwamba watu wengine hawapitii jambo hilo hilo. Unaweza kuripoti utapeli bila kutaja utambulisho na huna haja ya kutaja jina lako. Unaweza pia kuwasilisha ripoti kwa niaba ya mtu mwingine.
Hakikisha unakusanya taarifa maalum kuhusu ulaghai au utapeli:
- Tarehe, muda, na mahali pa tukio
- Majina na mawasiliano ya mtu au biashara inayohusika
- Maelezo ya ukiukaji
Ripoti kwa |
Aina ya utapeli |
---|---|
Utapeli wa mafao ya uhamiaji |
|
Utapeli wa uhamiaji |
|
Utapeli wa kesi inayoendelea mahakamani |
|
Utapeli wa usafirishaji haramu wa binadamu |
|
Barua pepe, tovuti, au akaunti za mitandao ya kijamii zinazotiliwa shaka zinazodai kuwa zinahusika na USCIS |
|
Utapeli wa jumla |
|
Pesa au mali iliyopotea |
|
Ulaghai |
|
Utapeli wa mtandaoni |
|
Udanganyifu na unyanyasaji wa mwajiri |
Zungumza na mwanafamilia au rafiki unayemwamini au shirika lako la wahamiaji ikiwa unahitaji msaada. Pata msaada zaidi ikiwa mtu anakutishia.
Kuwa makini na taarifa nyingine za uongo
Kuna taarifa nyingi za uongo zinazosambazwa, hasa kuhusu suala la uhamiaji. Jihadharini na taarifa za upotoshaji na zisizo kamili.
Upotoshaji mara nyingi huitwa habari za uwongo. Imekusudiwa kushawishi maoni yako. Taarifa isiyo kamili haikusudii kukupotosha lakini bado inakupa taarufa isiyo sahihi.
Vidokezo:
- Jihadhari na mahali ambapo habari na taarifa zako zinatoka
- Kuwa makini na taarifa unazopata kwenye mitandao ya kijamii
- Angalia vyanzo halisi ndani ya makala au chapisho
- Soma kuhusu mwandishi na shirika ili kuona kama ni wa kuaminika
- Thibitisha taarifa katika chanzo kingine
Taarifa kwenye ukurasa huu inatoka FTC, USCIS, DOJ, USA.gov, na vyanzo vingine vinavyoaminika. Tunakusudia kutoa taarifa rahisi kueleweka ambazo zinarekebishwa mara kwa mara. Taarifa hii sio ushauri wa kisheria.